Saturday, October 6, 2012

WANAFUNZI 255 WASHINDWA KUHITIMU MASOMO YAO




Wanafunzi 255 hawakufanya mtihani
Na Magreth Chaba
Wanafunzi 255 hawakufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu katika wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo tatizo la mimba na utoro.
Afisa elimu wa Halmashauri hiyo Gidion Mwesiga aliyasema hayo jana wakati akizungumza na mwandishi  wa habari ofisini kwake.

Mwesiga alisema wanafunzi hao waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa 12,117 lakini waliofanya mtihani huo wiki iliyopita walikuwa 11,862 ambao ni sawa na asilimia 98 ya wanafunzi waliosajiliwa.

Alisena kuwa kati ya wanafunzi hao hawakufanya mtihani huo wa kuhitimu elimu ya msingi kutokana na baadhi yao kuwa watoro na baadhi kupata ujauzito na kuwapelekea kutohitimu masomo yao.
Alisema Halmashauri hiyo imeanza kuchukua hatua kwa kuwabana wazazi walimu waongeze usimamizi kwa wanafunzi ili kukabiliana na tatizo la utoro, mimba za utotoni, kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wanaume walio wapatia mimba wanafunzi hao.

Pia alisema kuwa wanafunzi watakaopata ujauzito na kushindwa kuwataja wahusika nao watachukuliwa hatua ni pamoja na wazazi walio  waozesha watoto wao kuwaachisha masomo kufikishwa mahakamani.

Aidha amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuhakikisha suala la elimu wanalipa kipaumbele kwakuchangia shughuli za ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu. 

Hata hivyo amewataka wananchi kushirikiana na serikali kwa dhati kupambana na vitendo vya ubakaji kwa watoto waliochini  ya umri  utoro na ajira za watoto wadogo majumbani ili kuhakikisha wanajenga jamii iliyo bora kielimu.

No comments:

Post a Comment