Monday, November 26, 2012

JWTZ LA TOA UFAFANUZI MLIPUKO NGARA




JWTZ LATOA UFAFANUZI MLIPUKO NGARA.

Na Magreth chaba ,Ngara
JESHI la wananchi wa Tanzania  JWTZ  kikosi cha Faru makao makuu ya  Tabora limetoa ufafanuzi juu ya msihndo mkubwa uliojitokeza wilayani ngara mkoani kagera na kusababisha baadhi ya wananchi kuyakimbia kwa muda makazi yao kwa kuhofia maisha kutokana na kile walichodai bomu lilidondoka kwenye kijiji cha Ruganzo wilayani humo.

Katika tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa Novemba 22 majira ya saa nane lilisababisha baadhi ya wakazi wa wilaya ya ngara kuishi kwa hofu kubwa kutokana kitu kisichofahamika kudondoka toka angani na kusababisha mshindo mkubwa mithili ya tetemeko la ardhi hali iliyopelekea baadhi ya nyumba kupata nyufa.

Kufuatia hali hiyo kiongozi wa kikosi cha JWTZ  Mnadhimu mkuu wa mafunzo  na utendaji wa kivita Brigedia ya Faru Kanali Simon Lali Hongoa amelazimika kutoa ufafanuzi wa kitu hicho baada ya wataalamu wa mabomu kufika kijiji cha Ruganzo kata ya Kibimba wilayani Ngara na kufanya uchunguzi wa kina baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kushindwa kubaini ni kitu gani pamoja na madhara yake.
Kanali Hongoa alikanusha vikali madai ya wananchi wa ngara kuwa kitu kilichodondoka wilayani humo kilikuwa ni bomu la kivita na kudai kuwa maneno hayo hayakuwa na ukweli wowote kwa kuwa kilichodondoka kilikuwa ni kipande cha setelaiti iliyokuwa ikisafiri angani na inahofiwa kiliishiwa nguvu na kudodoka  katika eneo hilo.

Aidha alidai kuwa uchunguzi wa kitaalamu umebainisha kuwa setelaiti hiyo haina madhara yoyote na wala haikutoka uelekeo wa nchi jirani zinazoendelea na migogoro ya kivita kama baadhi ya maelezo ya wananchi wa wilaya hiyo walivyodai.
Hangoa alisema pamoja na kutokuwepo madhara kila mwananchi anatakiwa kuchukua tahadhari ya kubeba vitu wasivyokuwa na uhakika navyo wakilenga kutaka kupata utajiri wa haraka ambao unaweza kuhatarisha maisha yao na jamii inayowazungukana sanjari na kuleta matatizo kwa taifa.
“Kila inapotokea mtu yeyote akaona kitu ambacho hana uhakika nacho usikichukue kwa masuala ya kupata dili utakuja kufa na kuua familia  ni bora ukatoa taarifa katika vyombo vya usalama”.Alisema Hongoa
 Alitoa mfano wa baadhi ya matukio kama hayo yaliyotokea hivi karibuni ambayo yalisababisha madhara makubwa kwa watoto  wilayani karagwe na Arusha na kusababisha  hasara kwa wazazi wao na hata taifa kwa kupoteza rasilimali watu ambao wangekuwa wazalishaji wa uchumi wa taifa.
Awali kabla  kikosi hicho kutoka Tabora hakijawasili wilayani Ngara kulifika kikosi  cha wataalamu wa kambi ya JWTZ Biharamulo lakini uchunguzi wao ulitia mashaka na kulazimika kutoa taarifa ngazi nyingine kwa ajili ya uchunguzi wa kina licha ya baadhi ya wananchi na wanafunzi wa shule ya sekondari ya kata ya kibimba kuonyesha utukutu wao kwa kukinyanyua kutoka kilikotua na kukipeleka jirani zaidi na  shule yao zaidi ya mita 500
Kitu hicho kizito kilidondoka usiku wa manane na kuzama nusu yake ardhini kwa ukubwa wa diameta 50 kilomita mbili nje ya uwanja wa ndege wa kijiji cha  Ruganzo ambapo baadhi ya raia  walidhani kuwa ni Kimondo,kilichodondoka na kusababisha mshindo mkubwa uliosikika wilaya nzima na  nchi za jirani.
Akihutubia wananchi Mwenyekiti wa kijiji cha Ruganzo  kata ya kibimba wilaya ya  Ngara mkoani Kagera Salvatori Mbanyi  alisema kuwa kitu hicho kilidondoka kutoka angani na mshindo wake kuwashtua wananchi na asubuhi yake kilionwa na watu karibu na mto Ruvubu unaopita kijiji humo kutoka mpakani mwa nchi ya Burundi kuelekea Rusumo mpakani mwa Ngara na Rwanda.
Mbanyi alisema kuwa mara baada ya wananchi kuona kilichosababisha mlipuko viongozi walipeleka taarifa kwa  jeshi la polisi pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ajili ya kupata maelekezo na ufafanuzi zaidi  ambapo kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ilianza kazi yake .
Alisema kadri masaa yalivyosogea asubuhi umbo lake liliongezeka na kutanuka kama vile kinataka kulipuka na baadaye hali hiyo iliisha na  baadhi ya wananchi  walianza kukisogelea na kukigusa  kisha  kujaribu kukihamisha huku  watoto na wanafunzi wakikinyofoa nyuzi zilizokifunika                  

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ngara Costantine Kanyasu alisema kutokana na kitu hicho kuanguka eneo la wilaya yake lilisababisha taharuki kubwa kwa wananchi ambapo baadhi yao waliamini kuwa ni kombora la masafa marefu lililorushwa kutoka kutokana na vita vinavyoendelea kwenye nchi ya DRC dhidi ya waasi wa 23 na majeshi la serikali.

Kamanda wa polisi mkoani kagera Philip Karangi aliwataka wananchi wa ngara kushilikiana na vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo kwa kutoa taarifa za kiusalama mapema ili kuondoa madhara yanayoweza kujitokeza badala ya baadhi ya wananchi kufanya kazi za kitaalamu zisizowahusu hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kutokana na uzembe.

Kikosi cha Brigedia ya Faru Makao makuu ya Tabora kinasimamia mikoa minane ya Kanda ya ziwa ikiwa ni Tabora,Shinyanga,Simiyu,Mara,Mwanza,Geita,Kagera na Kigoma.
                                                                          Mwisho.

No comments:

Post a Comment