Na
Magreth Chaba
Shahidi wa pili katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu Jimbo la Biharamulo Magharibi Saniha Kasimu (23) mkazi wa Runazi wilayani Biharamulo akiongozwa na wakili wa upande wa mlalamikaji Bw. Aaron Kabunga shahidi huyo amekili kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi.
Mbele ya jaji wa mahakama hiyo Jaji Richard Kibera wakili wa serikali Bw. Pius Mboya, wakishirikiana na wakili wa serikali Bw. Isimaily Majoti na wakili wa upande wa wajibu maombi Bw. Mathias Rweyemamu shahidi huyo wa pili alikili kujihusisha na vitendo vya rushwa, udanganyifu wakati wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na kukipa ushindi Chama cha CHADEMA.
Shahidi huyo Bi. Kasimu ameieleza mahakama kuwa katika kipindi hicho cha uchaguzi yeye alishiriki kama mgombea udiwani viti maalum, Kata ya Runazi, kupitia chama cha CHADEMA, pia alikuwa wakala wa usimamizi wa wapigaji kura Kata ya Nemba kupitia CHADEMA na alikuwa Katibu wa vijana tawi Kata ya Runazi na alikuwa akihamasisha vijana wadogo kujiandikisha kupiga kura kwa kuwapa pesa.
Pia shahidi huyo amesema kuwa wakati wa kampeni alikuwa akihamasisha vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura katika mikutano ya hadhara na alishiriki kampeni za nyumba kwa nyumba huku akitoa fedha ili kuwashawishi wananchi waweze kukipigia kura Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Amevitaja baadhi ya vijiji ambako alifika na kutoa rushwa hiyo kuwa ni kijiji cha Nyambale Kata ya Lusahunga hakumbuki kiasi alichotoa na alikuwa akitoa sh. 50,000/= kwa wanawake na vijana sh. 30,000/= na kijiji cha Migango Kata ya Runazi ambako hakumbuki alitoa fedha kiasi gani.
Shahidi huyo Bi. Kasimu pia amekili kuvuruga uchaguzi mkuu 2010 kwa kuhamasisha vijana wadogo chini ya miaka (18) kujiandikisha, pamoja na kutoa rushwa kwa wananchi kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU na amekili kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Aidha, shahidi huyo katika ushahidi ameieleza mahakama kuwa alikuwa akitoa rushwa hizo mchana na usiku na ameamua kutoa ushahidi huo si kwa chuki bali ni kukilekebisha chama na kusahihisha makosa yote na kiwe katika mstari mzuri. Na kuiomba mahakama imsamehe kwa makosa aliyoyatenda mwaka 2010 na yuko tayari kulipa faini ya makosa hayo.
Hata hivyo, shahidi huyo baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake alitiwa nguvuni na jeshi la polisi wilayani hapa.
No comments:
Post a Comment