KATIKA hatua
iliyo kinyume na kanuni,taratibu na sheria za utumishi wa umma,idara ya elimu
msingi wilayani Sengerema mkoani Mwanza,imeingia katika mgogoro mkubwa na baadhi
ya walimu kutokana na kuwapa uhamisho wa adhabu bila malipo baadhi yao kwa kile
kilichodaiwa wamekuwa wakijihusisha na masuala ya kisiasa kinyume na taratibu za
kazi.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu ndani ya
idara hiyo zilisema hatua hizo zimeanza kuchukuliwa kutokana na shinikizo la
madiwani wa ccm,ambao wamekuwa wakiwatuhumu walimu hao kujihusisha na siasa
mahali pakazi na wakati wa kazi,tuhuma ambazo zilifikishwa hadi kwa mkuu wa mkoa
wa Mwanza mhandisi,Evarist Ndikilo ambaye alitoa agizo kwa aliyekuwa mkuu wa
wilaya hiyo Elinas Pallangyo kuwachukulia hatua walimu hao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
kwa masharti ya majina yao yasiandikwe ,baadhi ya walimu
walisema kuwa wameshangazwa na hatua hiyo ya uongozi wa wa idara ya elimu
Sengerema kwa vile hakuna utaratibu unaoonyesha mwalimu au mtumishi kumhamisha
bila malipo.
‘’Kisheria sisi..hatupaswi kuhama bila
malipo…kama wanaudhibitisho kweli walikutukuta tunajihusisha na siasa madarasani
ama ofisini..watupeleke mahakamani,mimi sihami,na kama kunifukuza kazini
wanifukuze,niko ladhi kwenda kulima au kuuza mitumba na sio kujihamisha
mwenyewe’’alisema mmoja wa walimu hao.
Ofisa utumishi wa halmashauri hiyo,Lusajo
Ngabo,alisema hatua zilizoanza kuchukuliwa na idara ya elimu msingi za
kuwahamisha walimu hao bila malipo kuwa ziko kinyume na utaratibu wa utumishi wa
umma,huku akipinga kuwa hakuna uhamisho unaoitwa uhamisho wa adhabu .
Alisema kuwa hatua zilioanza kuchukuliwa na idara
hiyo ni kinyume cha kanuni,sheria na taratibu za utumishi wa umma za kumhamisha
mtumishi bila kumlipa stahiki zake ikiwa ni pamoja na fedha za usumbufu,huku
akipinga kauli ya ofisa elimu msingi anayedai kuwa uhamisho huo ni uhamisho wa
adhabu.
Alisema sheria namba 50 na 51 ya utumishi wa umma
ya mwaka 2003 inafafanua kuwa mtumishi wa umma anaruhusiwa kuwa mwanasiasa na
kwamba ana uhuru wa kuwasiliana na viongozi wa chama chake isipokuwa hapaswi
kuiba nyaraka za serikali na kuzipeleka kwa viongozi wake wa chama.
‘’Mtumishi hazuiriwi kuwa mwanasiasa…isipokuwa
hatakiwi kujihusisha na siasa wakati wa kazi na mahali pa kazi,lakini anaweza
kuwa na ushabiki wa chama chochote kile…kwa maana hiyo hatua hizi zilizoanza
kuchukuliwa ni kinyume cha sheria za utumishi wa umma..na hakuna uhamisho
unaoitwa uhamisho wa adhabu’’alisema Ngabo.
Hata hivyo ofisa utumishi huyo alikiri kupata
taarifa za kuwepo kwa uhamisho huo na kumtaka ofisa elimu Juma Mwanjombe kumpa
nakala ya barua za uhamisho huo jambo ambalo halijatekelezwa na hivyo kupinga
kuwa hakuna uhamisho wa adhabu unaotokana na ushabiki wa kisiasa.
Aliongeza kuwa mtumishi atachukuliwa hatua kama
atashiriki siasa wakati na mahala pa kazi na si vinginevyo na anapobainika
kufanya hivyo atashitakiwa kwa kosa la kujihusisha na siasa wakati na mahala pa
kazi,wala adhabu yake sio uhamisho.
Akizungumzia agizo la mkuu wa mkoa wa Mwanza
alilolitoa mei 8,mwaka huu kwa aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Sengerema Elnasi
Pallangyo,la kuhakikisha anawabaini walimu wanaojihusisha na siasa,ofisa
utumishi alisema mkuu wa mkoa ni mwanasiasa na kwamba kila hatua huhukuliwa kwa
kufuata sheria kwani agizo hilo alipaswa kulitoa kwa maandishi ya barua.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya ofisa
elimu mei 17,mwaka huu kuwaandikia barua za uhamisho walimu 27 kati yao walimu
saba wanadaiwa kujihusiha na siasa,huku walimu wengine 20 wanasemekana kuishi
nje na vituo vyao vya kazi.
Uchunguzi uliofanywa na MWANDISHI wa habari hizi umebaini
kuwa bali na walimu hao kukiri kuzipokea barua hizo za uhamisho wamegoma kuhama
kwenda kwenye vituo walivyopangiwa hadi watakapolipwa fedha za uhamisho,ambapo
wamepinga kauli ya ofisa elimu ya kwamba wao wanajihusisha na siasa.
Kaimu
mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema ambaye pia ni ofisa elimu
msingi wilaya hiyo Juma Mwanjombe akizungumzia sakata hilo alisema hilo ni agizo
la madiwani na kwamba hawezi kulipuuza huku akisisitiza kwamba mwalimu
atakayeshindwa kutekeleza atasimamishiwa mshahara wake.
Alisema hatua hizo ni kufuatia madiwani kubaini
kuwa kuna baadhi ya walimu wamekuwa wakitoroka vipindi vyao vya masomo na kwenda
kwenye vijiwe vya kahawa na kuanza kuzungumzia masuala ya siasa kinyume na
sheria za utumishi wa umma.
MWISHO
No comments:
Post a Comment