Monday, October 1, 2012

BASI LATEKETEA 9 WAJERUHIWA

Na Magreth Chaba
BIHARAMULO


ABIRIA kadhaa wanasadikika kufariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuteketea kwa moto katika kijiji cha Nyantakala wilayan Biharamulo mkoani Kagera.
Ajali hiyo imetokea saa 4:30 asubuhi imelihusisha basi la kampuni ya Adventure lenye namba T 294 ABD aina ya scania ambalo lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda mkoani Kigoma.
Majeruhi wa ajali wamelazwa katika hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo na kwamba kati ya majeruhi tisa wawili kati yao akiwe ajenti wa basi hilo Dotto Tryphone[30]mkazi wa Nyakanazi wamevunjika miguu wakati wakijinasua kutoka kwenye basi hilo baada ya kushika moto.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera,Paulo Alex Kalangi alipotafutwa kuzungumzia ajali alisema atatoa taarifa hizo baadaye kwa kuwa alikuwa kwende ufuatiliaji wa ajali hiyo.
Aidha Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo wakiwemo majeruhi wamesema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya basi hilo kufika kwenye tuta  la kuzuia mwendo kasi  walishitukia moshi unatokea ndani ya basi kabla ya kushika moto na kuanza kuteketea.
‘’Basi lilikuwa kwenye mwendo wa kawaida lakini lilipofika kwenye bamzi[tuta]tulishtukia basi linashika moto ,tukaanza kuruka,kuna baadhi ya wenzetu hasa watoto na wazee huenda wameteketea kwenye basi hilo,maana basi limewaka na kuwa majivu kabisa’’alisema Tryphone.
Akizungumzia ajali hiyo kwa shida akiwa katika wodi ya majeruhi Tryphone alisema huenda chanzo cha kulipuka kwa basi hilo kinatokana na hitilafu katika mfumo wake wa umeme.
Dereva wa basi hilo ambaye hakutambulika jina lake haijajulikana kama alikimbia au aliteketea kwenye basi hilo mara baada ya kutokea ajali hiyo. 
Mganga mkuu msaidizi wa hospitali hiyo Gabriel Mashauri amesema amepokea majeruhi tisa na kwamba saba kati yao walikuwa katika hali mbaya lakini bado wanaendelea kupatiwa matibabu.
Amewataja majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo ni Phinihas Elias[37]mwalimu wa shule ya sekondari Shamaliwa Igoma jijini Mwanza,Pius John[21],Msigwa Isaya[18]mwanafunzi wa shule ya sekondari Kigoma,Johary Chapa[23]Mkazi wa Kwimba mkoani MwanKza,Josephina Ngereza[46],Rashidi Mahonda[48] na Eles Ngereza[60] wote wakiwa wameungua moto sehemu mbalimbali za miili yao.
Waliovunjika miguu katika ajali hiyo wakati wakijinasua kutoka ndani ya basi hilo wametambulika kwa majina ya  Dotto Tryphone[30]mkazi wa Nyakanazi na Zainabu Issa ambao wote wamevunjika miguu ya kushoto.


 

No comments:

Post a Comment