Na Magreth
Chaba,Chato.
ASKARI wa kituo kidogo cha Polisi cha Buziku wilayani
Chato mkoani Geita wamekumbwa na kashfa kubwa baada ya kutuhumiwa kuwakamata na
kuwatesa wananchi wawili waliokuwa wamelala kwenye nyumba ya wageni ya Buziku
Hill Guest House hali iliyosababisha mmoja wao kupoteza maisha.
Tukio hilo limetokea Oktoba 3 mwaka huu majira ya saa
5;30 usiku wakati wananchi hao wakiwa wamejifungia ndani ya vyumba vyao
wakiendelea kunywa pombe(Bia) ambapo askari polisi walifika eneo hilo na
kuwaamuru kufungua milango yao kwa lengo la kuwafanyia upekuzi.
Baada ya wananchi hao kukaidi amri ya polisi,askari hao
walilazimika kutumia nguvu na kufanikiwa kuvunja milango ya vyumba hivyo kisha
kuanza kuwaadhibu watu hao kabla ya kuwapeleka kwenye kituo kidogo cha polisi
kilichopo kwenye kata hiyo.
Aidha ameelezwa kuwa baada ya kipigo kikali vijana hao
walipelekwa kwenye kituo hicho cha polisi na kabla ya kuhojiwa hali zao kiafya
zilibadilika ghafra na kulazimika kuwakimbiza kwenye Kituo cha afya cha Bwanga
kwaajili ya matibabu lakini kutokana na kuonekana mahututi zaidi walikimbizwa
hospitali ya wilaya ya chato.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Paulo Kasabago
amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa askari wake walifika eneo la tukio
baada ya kuelezwa na raia mwema kuwa kuna watu wanaosadikiwa ni majambazi
kutokana na mazungumzo waliyokuwa nayo wakati wakinywa pombe nje ya guest hiyo
kabla ya kuingia ndan ya vyumba vyao kulala.
Ameeleza kuwa baada ya askari wake kuingia ndani kwa
lengo la kuwakamata watuhumiwa na kuwafanyia upekuzi,mmoja wa watuhumiwa hao
alimkwida koo askari PC Mwidin hali iliyosababisha askari wenzake kutumia nguvu
kubwa ili kumsuru mwenzao kujeruhiwa.
Amesema baada ya kufanikiwa kuwatoa ndani ya vyumba vyao
na kabla ya kuwafikisha kituoni,kundi kubwa la wananchi waliokuwa wanatoka
kutazama soka la ulaya kwenye moja ya ukumbi uliopo kijijini hapo walifika
kwenye tukio na kuanza kuwasaidia polisi kuwapeleka watuhumiwa hao lakini
kutokana na kukataa kata kata wananchi waianza kuwaadhibu huku mkuu wa kituo
hicho cha polisi akilazimika kuwazuia.
Baada ya kumalizika upekuzi wa askari walifanikiwa kukuka
kiasi cha shilingi laki 5 ndani ya chumba kimoja na kingine walikuta kiroba cha
mfuko uliokuwa na mawe yanayosadikiwa kuwa ni ya dhahabu pamoja na chupa moja ya
pombe aina ya Bia.
Kadhalika wakati watuhumiwa hao wakiendela kupata
matibabu kwenye hospitali ya wilaya ya chato,mmoja wao alifariki dunia wakati
akiendelea kutibiwa.
Kasabago amemtaja aliyepoteza maisha kuwa ni Gilbert
Ntabonwa mkazi wa kijiji cha Kakeneno na mzaliwa wa Kibondo mkoani Kigoma huku
majeruhi mwingine David Vyamana hali yake ikiendelea vizuri.
Kufuatia hali hiyo jeshi hilo linawashikilia askari wake
wanne kwaajili ya uchunguzi kutokana na kutuhumiwa na kuhusika na tukio la
kujeruhi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kwamba uchunguzi utakapo kamilika
hatua za kisheria zitachukuliwa.
Amewataja askari
wanaoshikiliwa kuwa ni OCS wa kituo hicho Sajent Raulens Bendera,PC Mwidin,PC
abdalah na PC Yusuph wote wakiwa ni askari wa kituo kidogo cha Buziku.
Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Chato Dk Pius
Buchukundi amekiri mmoja wa majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kufariki
dunia wakati akiendelea na matibabu.
Amesema uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa marehemu
alikuwa amejeruhiwa vibaya kutokana na kipigo hali iliyosababisha damu kuvujia
ndani ya mwili na hivyo kupelekea mauti hayo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment