WANAFUNZI 138 wa
kidato cha nne katika shule ya sekondari Senga wilayani
Geita,wamekatisha masomo yao kutokana na mwamko mdogo wa elimu na kipato
duni kinachowakabili wazazi na walezi wao.
Mkuu wa shule
hiyo,Mwalimu Magoma Komesi,amesema hayo kwenye mahafari ya tano ya
kidato cha nne yaliyofanyika juzi wakati akisoma taarifa ya shule hiyo
kwa mgeni rasim meneja wa Benki ya NMB wilaya ya Geita Bw.Mdasi Kalema.
Mwalimu
Komesi amesema kuwa kati ya wanafunzi 241 kati yao wavulana 177 na
wasichana 64 waliosajiliwa kujiunga na masomo shuleni hapo mwaka 2009 ni
wanafunzi 103 kati yao wavulana 85 na wasichana 18 ndiyo wamefanikiwa
kufika kidato cha nne na kusajiliwa kufanya mtihani wa Taifa mwaka huu.
Amesema
tatizo hilo linatokana na wazazi na walezi kuishi kwa kutegemea kilimo
na uvuvi ambapo kutokana na hali ya hewa kubadilika na kujitokeza ukame
wazazi hukosa mazao ya kuuza ili kuwaendeleza watoto wao,ambao kutoka na
hali hiyo baadhi yao wameamua kuoa na kuolewa.
Hata hivyo katika
risala ya wahitimu hao iliyosomwa na mwanafunzi Waziri Sabaganga
wamesema shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa walimu ,vyumba vya
madarasa na maabara hali ambayo imekuwa ikiwasababishia kutofanya vizuri
katika mitihani yao na hivyo kuiomba serikali kuweka mikakati madhubuti
ya kuondoa tatizo hilo.
Kwa upande wake mgeni Rasmi katika
mahafari hao meneja wa NMB Geita Bw.Kalema amewataka wanafunzi hao
kujiepusha na vitendo viovu kama matumizi ya dawa za kulevya na ngono
ambavyo vinaweza kukatisha ndoto zao kuendelea na elimu ya juu kwa
manufaa ya familia zao na Taifa kwa ujumla.
MWISHO
No comments:
Post a Comment