Saturday, October 6, 2012

WANAFUNZI 255 WASHINDWA KUHITIMU MASOMO YAO




Wanafunzi 255 hawakufanya mtihani
Na Magreth Chaba
Wanafunzi 255 hawakufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu katika wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo tatizo la mimba na utoro.
Afisa elimu wa Halmashauri hiyo Gidion Mwesiga aliyasema hayo jana wakati akizungumza na mwandishi  wa habari ofisini kwake.

Mwesiga alisema wanafunzi hao waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa 12,117 lakini waliofanya mtihani huo wiki iliyopita walikuwa 11,862 ambao ni sawa na asilimia 98 ya wanafunzi waliosajiliwa.

Alisena kuwa kati ya wanafunzi hao hawakufanya mtihani huo wa kuhitimu elimu ya msingi kutokana na baadhi yao kuwa watoro na baadhi kupata ujauzito na kuwapelekea kutohitimu masomo yao.
Alisema Halmashauri hiyo imeanza kuchukua hatua kwa kuwabana wazazi walimu waongeze usimamizi kwa wanafunzi ili kukabiliana na tatizo la utoro, mimba za utotoni, kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wanaume walio wapatia mimba wanafunzi hao.

Pia alisema kuwa wanafunzi watakaopata ujauzito na kushindwa kuwataja wahusika nao watachukuliwa hatua ni pamoja na wazazi walio  waozesha watoto wao kuwaachisha masomo kufikishwa mahakamani.

Aidha amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuhakikisha suala la elimu wanalipa kipaumbele kwakuchangia shughuli za ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu. 

Hata hivyo amewataka wananchi kushirikiana na serikali kwa dhati kupambana na vitendo vya ubakaji kwa watoto waliochini  ya umri  utoro na ajira za watoto wadogo majumbani ili kuhakikisha wanajenga jamii iliyo bora kielimu.

Wednesday, October 3, 2012

ASKARI NA KASHFA NZITO

Na Magreth Chaba,Chato.

ASKARI wa kituo kidogo cha Polisi cha Buziku wilayani Chato mkoani Geita wamekumbwa na kashfa kubwa baada ya kutuhumiwa kuwakamata na kuwatesa wananchi wawili waliokuwa wamelala kwenye nyumba ya wageni ya Buziku Hill Guest House hali iliyosababisha mmoja wao kupoteza maisha.

Tukio hilo limetokea Oktoba 3 mwaka huu majira ya saa 5;30 usiku wakati wananchi hao wakiwa wamejifungia ndani ya vyumba vyao wakiendelea kunywa pombe(Bia) ambapo askari polisi walifika eneo hilo na kuwaamuru kufungua milango yao kwa lengo la kuwafanyia upekuzi.

Baada ya wananchi hao kukaidi amri ya polisi,askari hao walilazimika kutumia nguvu na kufanikiwa kuvunja milango ya vyumba hivyo kisha kuanza kuwaadhibu watu hao kabla ya kuwapeleka kwenye kituo kidogo cha polisi kilichopo kwenye kata hiyo.

Aidha ameelezwa kuwa baada ya kipigo kikali vijana hao walipelekwa kwenye kituo hicho cha polisi na kabla ya kuhojiwa hali zao kiafya zilibadilika ghafra na kulazimika kuwakimbiza kwenye Kituo cha afya cha Bwanga kwaajili ya matibabu lakini kutokana na kuonekana mahututi zaidi walikimbizwa hospitali ya wilaya ya chato.

Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Paulo Kasabago amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa askari wake walifika eneo la tukio baada ya kuelezwa na raia mwema kuwa kuna watu wanaosadikiwa ni majambazi kutokana na mazungumzo waliyokuwa nayo wakati wakinywa pombe nje ya guest hiyo kabla ya kuingia ndan ya vyumba vyao kulala.

Ameeleza kuwa baada ya askari wake kuingia ndani kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa na kuwafanyia upekuzi,mmoja wa watuhumiwa hao alimkwida koo askari PC Mwidin hali iliyosababisha askari wenzake kutumia nguvu kubwa ili kumsuru mwenzao kujeruhiwa.

Amesema baada ya kufanikiwa kuwatoa ndani ya vyumba vyao na kabla ya kuwafikisha kituoni,kundi kubwa la wananchi waliokuwa wanatoka kutazama soka la ulaya kwenye moja ya ukumbi uliopo kijijini hapo walifika kwenye tukio na kuanza kuwasaidia polisi kuwapeleka watuhumiwa hao lakini kutokana na kukataa kata kata wananchi waianza kuwaadhibu huku mkuu wa kituo hicho cha polisi akilazimika kuwazuia.

Baada ya kumalizika upekuzi wa askari walifanikiwa kukuka kiasi cha shilingi laki 5 ndani ya chumba kimoja na kingine walikuta kiroba cha mfuko uliokuwa na mawe yanayosadikiwa kuwa ni ya dhahabu pamoja na chupa moja ya pombe aina ya Bia.

Kadhalika wakati watuhumiwa hao wakiendela kupata matibabu kwenye hospitali ya wilaya ya chato,mmoja wao alifariki dunia wakati akiendelea kutibiwa.

Kasabago amemtaja aliyepoteza maisha kuwa ni Gilbert Ntabonwa mkazi wa kijiji cha Kakeneno na mzaliwa wa Kibondo mkoani Kigoma huku majeruhi mwingine David Vyamana hali yake ikiendelea vizuri.

Kufuatia hali hiyo jeshi hilo linawashikilia askari wake wanne kwaajili ya uchunguzi kutokana na kutuhumiwa na kuhusika na tukio la kujeruhi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kwamba uchunguzi utakapo kamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.

Amewataja askari wanaoshikiliwa kuwa ni OCS wa kituo hicho Sajent Raulens Bendera,PC Mwidin,PC abdalah na PC Yusuph wote wakiwa ni askari wa kituo kidogo cha Buziku.

Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Chato Dk Pius Buchukundi amekiri mmoja wa majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kufariki dunia wakati akiendelea na matibabu.

Amesema uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa marehemu alikuwa amejeruhiwa vibaya kutokana na kipigo hali iliyosababisha damu kuvujia ndani ya mwili na hivyo kupelekea mauti hayo.

Mwisho.

Tuesday, October 2, 2012

HATIMAYE ATARAJIWA KUZIKWA RASMI



Na
Magreth Chaba
BUKOBA
Zikiwa zimesalia siku 3 kuuzika rasmi mwili Kardinali wa kwanza Afrika na askofu wa kwanza Mwafrika Mwadhama Laurian Rugambwa ambaye alizikwa kwa muda katika kanisa la Kashozi mwaka 1997, hatimaye atazikwa rasmi katika kanisa kuu jimbo Katoliki la Bukoba, baada ya ukarabati wake kukamilika.

Askofu msaidizi wa jimbo Katoliki la Bukoba Methodius Kilaini alisema kuwa maamuzi ya marehemu Rugambwa kuzikwa Kashozi yalitokana na kanisa hilo alilochagua kuzikwa kuwa katika ukarabati tangu mwaka 1996.

Askofu Kilaini alisema kuwa mazishi hayo rasmi yatafanyika Oktoba 6 mwaka huu, siku ambayo pia itakuwa ni kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Kardinali Rugambwa ambaye alizaliwa mwaka 1912.

“Masalia  ya Kardinali Rugambwa yatahamishwa rasmi siku hiyo kutoka kanisa Katoliki la Kashozi, tutasherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwake, lakini pia siku hiyo Kanisa Katoliki jimbo la Bukoba litatabalukiwa” alisema.

Alisema kitendo hicho ni kumbukumbu  nzuri kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla kutokana na kuwa Kardinali wa kwanza Afrika na Askofu wa kwanza Mwafrika,  hivyo  wanategemea kupata wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, na kwamba baada ya mazishi hayo kanisa hilolitaanza kutumika


Alisema kuwa baada ya shughuli hizo, kanisa Katoliki jimbo la Bukoba linataendelea kutumika kwa ibada za kawaida, ili  kuwaondolea waamini wao adha ya kusalia katika holi.

“Tunaendelea kuhamasisha waamini wetu wachangie fedha kwa ajili ya kumalizia sehemu ya ujenzi iliyobaki, lakini pia wachangie sherehe hizo ili ziweze kufanyika kwa ufanisi” alisema Askofu Kilaini.

Akizungumzia historia ya Kardinali Rugambwa alisema kuwa alipewa Upadre mwaka 1943,  mwaka 1952 akapewa Uaskofu, mwaka 1960 akawa Kardinali na mwaka 1969 akawa Askofu Mkuu Dar-Es-Salaam  hadi alipostaafu mwaka 1992.

Akigusia kidogo aliyoyafanya Kardinali Rugambwa ambayo baadhi yake yanawafanya watu waweke  kumkumbuka, Askofu Kilaini alisema kuwa alianzisha kanisa kuu jimbo la Bukoba, alileta seminari kuu ya Ntungamo na alijenga shule ya sekondari Rugambwa.

Mengine ni ujenzi wa hospitali ya Mugana, kuanzisha vikoba kwenye parokia, kuanzisha seminari ndogo ya Visiga na kuanzisha seminari kuu ya Segerea iliyoko Dar-es-Salaam.

Mwisho.

AFYA ZA MAJERUHI WA BASI LILO TEKETEA KWA MOTO ZAENDELEA VIZURI



Na

Magreth chaba


BIHARAMULO

HALI za majeruhi waliolazwa katika Hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo kutokana na ajali ya basi lilliloteketea kwa moto katika kijiji cha Nyantakala wilayani Biharamulo mkoani Kagera zimeelezwa kuendelea vizuri huku mmoja kati yao akiwa ameruhusiwa.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo Grasimus Sebuyoya amesema hali zao zinaendelea vizuri ikilinganishwa na hali zao walipokuwa wanapokelewa katika hospitali hiyo.
Majeruhi aliyeruhusiwa ametambulika kwa jina la Msigwa Isaya[22]mkazi wa Katoro mkoani Geita ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Kigoma.
 Majeruhi wanaoendelea kupata matiobabu katika hospitali hiyo ni Phinihas Elias[37]mwalimu wa shule ya sekondari Shamaliwa Igoma jijini Mwanza,Pius John[21]askari wa JWT kikosi cha 24 kj Kigoma,Johary Chapa[23]Mkazi wa Kwimba mkoani Mwanza,Josephina Ngereza[46]Kasulu ,Rashidi Mahonda[48]Kasulu  na Elies Ngereza[60]kazi wa kasulu wote wakiwa wameungua moto sehemu mbalimbali za miili yao.
Majeruhi wengine ni  Dotto Tryphone[30]mkazi wa Nyakanazi na Zainabu Issa(23)Mkazizi wa kigoma  ambao wote wamevunjika miguu ya kushoto.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 4:30 asubuhi na kulihusisha basi la kampuni ya Adventure lenye namba T 293 BDP Aina ya Nissani Diseal ambalo lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda mkoani Kigoma.
Aidha Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera,Philip Kalangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na hitilafu kwenye mfumo wa umeme na kuongeza kuwa uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea.
Hata hivyo kauli hiyo ya kamanda imetofautia na baadhi ya abiria wa basi hilo na mashuhuda wa ajali ambao walisema huenda baadhi yao waliungulia ndani ya basi hilo hasa watoto na wazee ambao walishindwa kujinusuru kutoka ndani ya basi hilo.
Kalangi alikanusha madai ya kutokea Vifo katika ajali hiyo isipokuwa mali zilizokuwemo ziliteketea kwa moto na kwamba abiria walionusurika katika ajali hiyo walisafirishwa na basi jingine.
                                             MWISHO.

Monday, October 1, 2012

WAGONJWA WATAABIKA,DUKALA DAWA LAFUGWA



      Na  Magreth Chaba.
MAMLAKA ya dawa na chakula Tanzania [TFDA]imefunga duka la madawa katika hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera baada ya duka hilo kuendeshwa bila ya kuwa na mfamasia wa kulihudumia.
Duka hilo limefungwa tangu Agosti mwaka huu na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo ambao kutokana na hali hiyo wamekuwa wakilazimika kwenda kununua dawa kwenye maduka ya watu binafsi.
Kwa mujibui wa mganga mkuu wa hospitali hiyo Dk.Grasimus Sebuyoya,alisema duka hilo limejengwa kwa thamani ya zaidi ya sh.12 milion na kwamba  limefungwa likiwa na dawa yenye thamani ya sh.30 millon.
Alisema kuwa uongozi wa hospitali hiyo ulifikia uamuzi wa kuanzisha duka hilo kutokana na bohari ya dawa nchini[msd] kushindwa kupeleka dawa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa ambao wamekuwa wakisumbuka kwenda kununua dawa hizo nje ya hospitali hiyo.
Pia,Dk.Sebuyoya alisema lengo la kuanzisha duka hilo ilikuwa kusaidia wagonjwa waliojiunga katika mifuko ya bima ya afya CHF na NHIF kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wa kutafuta dawa Kutokana na uhaba wa dawa kutoka Msd unaoikabili hospitali hiyo.
Alisema mamlaka ya dawa na chakula[TFDA]ilifunga duka hilo kutokana na kukosa mfamasia wa kulisimamia.
‘’Tulipolianzisha tulitegemea mfamasia wa halmashauri atakuwa msimamizi wa hilo duka lakini imekuwa tofauti,tulivyokuwa tumetarajia na sisi hapa hatuna mfamisia wa kulisimamia duka hilo,mpango uliopo tunatafuta mfamisia Atakayekithi kiwango ili alisimamie,tuendeleze huu mradi wetu’’alisema Dk.Sebuyoya.
Aidha Dk.Sebuyoya aliongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo makundi maalumu hususa ni akina mama wajawazito,watoto chini ya umri wa miaka 5,wazee na watu wenye magonjwa sugu wamekuwa wakilazimika kununua dawa kwenye maduka ya watu binafsi kinyume na tamko serikali la kutoa kuhuduma bure kwao.
‘’Serikali inasema tutoe huduma kwa makundi hayo bure,lakini inashindikana,maana bohari wana muda mrefu hawaleti dawa kwa maana hiyo tuna tatizo kubwa sana la ukosefu wa madawa na sisi tuliamua kuanzisha duka hili ili tuwasaidie wagonjwa wawe wanapata dawa karibu’’
Alisema hosiptali hiyo haijapokea dawa kutoka bohari ya Taifa tangu mwezi wa tatu mwaka huu na kwamba hali hiyo imekuwa ikiwalazimu wagongwa wanaofika katika hospitali hiyo wakiwemo watoto chini ya miaka mitano,wajawazito,na wazee kwenda kununua dawa hizo mitaani.
                                                                      MWISHO.                                                                   

BASI LATEKETEA 9 WAJERUHIWA

Na Magreth Chaba
BIHARAMULO


ABIRIA kadhaa wanasadikika kufariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuteketea kwa moto katika kijiji cha Nyantakala wilayan Biharamulo mkoani Kagera.
Ajali hiyo imetokea saa 4:30 asubuhi imelihusisha basi la kampuni ya Adventure lenye namba T 294 ABD aina ya scania ambalo lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda mkoani Kigoma.
Majeruhi wa ajali wamelazwa katika hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo na kwamba kati ya majeruhi tisa wawili kati yao akiwe ajenti wa basi hilo Dotto Tryphone[30]mkazi wa Nyakanazi wamevunjika miguu wakati wakijinasua kutoka kwenye basi hilo baada ya kushika moto.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera,Paulo Alex Kalangi alipotafutwa kuzungumzia ajali alisema atatoa taarifa hizo baadaye kwa kuwa alikuwa kwende ufuatiliaji wa ajali hiyo.
Aidha Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo wakiwemo majeruhi wamesema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya basi hilo kufika kwenye tuta  la kuzuia mwendo kasi  walishitukia moshi unatokea ndani ya basi kabla ya kushika moto na kuanza kuteketea.
‘’Basi lilikuwa kwenye mwendo wa kawaida lakini lilipofika kwenye bamzi[tuta]tulishtukia basi linashika moto ,tukaanza kuruka,kuna baadhi ya wenzetu hasa watoto na wazee huenda wameteketea kwenye basi hilo,maana basi limewaka na kuwa majivu kabisa’’alisema Tryphone.
Akizungumzia ajali hiyo kwa shida akiwa katika wodi ya majeruhi Tryphone alisema huenda chanzo cha kulipuka kwa basi hilo kinatokana na hitilafu katika mfumo wake wa umeme.
Dereva wa basi hilo ambaye hakutambulika jina lake haijajulikana kama alikimbia au aliteketea kwenye basi hilo mara baada ya kutokea ajali hiyo. 
Mganga mkuu msaidizi wa hospitali hiyo Gabriel Mashauri amesema amepokea majeruhi tisa na kwamba saba kati yao walikuwa katika hali mbaya lakini bado wanaendelea kupatiwa matibabu.
Amewataja majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo ni Phinihas Elias[37]mwalimu wa shule ya sekondari Shamaliwa Igoma jijini Mwanza,Pius John[21],Msigwa Isaya[18]mwanafunzi wa shule ya sekondari Kigoma,Johary Chapa[23]Mkazi wa Kwimba mkoani MwanKza,Josephina Ngereza[46],Rashidi Mahonda[48] na Eles Ngereza[60] wote wakiwa wameungua moto sehemu mbalimbali za miili yao.
Waliovunjika miguu katika ajali hiyo wakati wakijinasua kutoka ndani ya basi hilo wametambulika kwa majina ya  Dotto Tryphone[30]mkazi wa Nyakanazi na Zainabu Issa ambao wote wamevunjika miguu ya kushoto.