Monday, May 14, 2012

VIKONGWE WAUWAWA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

Na.Magreth Chaba
Geita.
WANANWAKE wanne ambao ni vikongwe wameuawa kwa kupigwa kwa mawe kisha miili yao kuteketezwa kwa moto na wananchi katika kijiji cha Lwezera wilayani Geita,mkoani Geita,kutokana na imani za kishirikina baada ya wananchi hao kuwatuhumu vikongwe hao kufuga fisi kwenye makazi yao.

Pia familia za vikongwe hao vimeachwa bila makazi baada ya nyumba zao zaidi ya 15 za vikongwe hao zimeteketezwa kwa moto na wananchi hao zaidi ya 1,000 ambao walikuwa wamekusanyikana   baada ya kuanzisha msako wa kila kaya pale inapongundulika kuwa anaishi kikongwe.

Mauaji ya vikongwe hao yametokea siku moja baada ya kutokea tukio la mtoto Diana Salu[5]mwanafunzi wa darasa la awali mkazi wa kijijini hapo kunyakuliwa na fisi akiwa na wenzake wakati wakitokea kibandani kununua mafuta ya taa waliyoagizwa na wazazi wake majira ya saa 2:30.

Baada ya mtoto huyo kunyakuliwa na fisi,watoto wenzake walienda kutoa taarifa nyumbani na kijihada za kumtafuta mtoto huyo  kwa kushirikia na wananchi wa kijiji hicho hazikufanikiwa hadi maiti yake ilipoonekana kesho yake[mei 8]ikiwa kwenye uwanja wa shule ya msingi Lwezera ikiwa imenyofolewa utumbo na mguu wa kushoto.

Kwa mujibu wa ofisa mtendaji wa kata ya Lwezera ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya kata Fransice Kadilo,alisema tukio hilo la mtoto kuliwa na fisi lilitokea mei 7,mwaka huu,wananchi waliwatuhumu vikongwe hao kufuga fisi hao waliosababishaa kifo cha mtoto Diana Salu.

‘’Walipokuta maiti ya mtoto huyo..ikiwa kwenye uwanja huo..walikuwa wengi ndipo walianza kufanya vurugu hizo za kuwapiga vikongwe na miili yao kuichoma moto,baadaye nilipiga simu polisi,wakawa wamefika eneo la tukio na kuthibiti hizo vurugu’’

Kundi hilo la wananchi baada ya kuwa limetoka uwanjani kushuhudia maiti ya mtoto huyo,lilianza msako wa kila nyumba na  kufanya mauaji hayo kwa kutumia mawe na silaha za jadi yakiwemo mapanga na marungu na nyumba 15 za vikongwe hao na wengine kuziteketeza kwa moto.

Ofisa mtendaji huyo aliwataja Vikongwe waliouawa katika tukio kwa majina ya Kulwa Mashana[65],Laurencia Bangili[62],Ester Konya[55] na Rozi Mabeshi[42]ambao wote ni wakazi wa kijiji hizcho cha Lwezera.

Katika tukio hilo vikongwe  wengine  wanane wamenusurika baada ya kuyakimbia makazi yao kwenda kusikojulikana mara baada ya kuona wananchi wamecharuka kwa hofu ya kushambuliwa na kuuawa.

Mkuu wa wilaya ya Geita Philimon Shelutete aliyefika eneo la tukio hilo mbali na kuwaonya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi,alilitaka jeshi la polisi lililokuwa katika eneo hilo kuzuia vurugu hizo,kufuatilia kwa kina chanzo cha vurugu hizo zilizogharimu maisha ya vikonwe hao na kulitaka kuwachukulia hatua waliohusika katika mauaji hayo.

Kauli hiyo ya mkuu wa wilaya imekuja wakati kukidaiwa kuwa idadi kubwa ya wananchi wa eneo hilo wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa hofu ya kukumbwa na mkono wa sheria kuhusiana na mauaji hayo.

Hilo ni tukio la pili kutokea wilayani Geita,ambapo tukio kama hilo liliwahi kutokea katika kijiji cha Rwamgasa baada ya vikongwe watatu kuuawa kwa kupigwa kwa mawe na miili yao kuteketezwa kwa moto huku nyumba zao zikiharibiwa kwa kuchomwa na moto.